KTN’s Mohammed Ali Open Letter to President Uhuru

After fateful events of Tana River, Baragoi, Westgate and most recently Mpeketoni, all in just under one year, KTN’s leading investigative reporter, Mohammed Ali has written to the President seeking answers.

He writes;

Rais,

Habari ya siku nyingi?

Jina langu ni Mohammed Ali, mwandishi wa habari ya runinga ya KTN. Mara ya mwisho kuonana naye ilikua wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita huko Mombasa katika shule ya msingi ya Khadija. Ulikua mchangamfu kando na ahadi chungunzima kwa Wakenya. Ahadi za tarakilishi za bure kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, kutoa nafasi za kazi milioni moja kila mwaka kwa vijana, kuekeza katika usalama wa kitaifa miongoni mwa ahadi zingine. Lakini, kwa hivi sasa bwana rais nahofia ahadi hizo zimekua tasa.

Barua yangu inaanza na maswala ya usalama ambayo nimeyapa kipau mbele.

Kwanza kabisa nauliza, “Uko wapi? Hatukuoni bwana Rais.”

Wakenya wanashabuliwa kila mara na kuuliwa kinyama. Walioponea wamebagi na vilema vya maisha.

Shambulizi la Westgate na ahadi ya serikali yako zilionekana kama hekaya za Abunuasi. Uliowapa majukumu ya kutulinda wako wapi? Kuanzia Mkurugenzi wa NIS, Michael Gichangi, Inspekta Jenerali wa Polisi, David Kimaiyo, Mkurugenzi wa CID, Ndegwa Muhoro, Kamanda wa GSU, Kitili Mboya, Waziri wa Usalama wa Ndani, Joseph Ole Lenku na Mkuu wa Majeshi, Julius Waweru Karangi.

Ukweli wa mambo ni kwamba Wakenya wanahisi kuwa nyote mmelala.

Usalama umegeuzwa na kuwa mchezo wa tufe. Tumejisahau kiasi cha hata kuonyesha siri zetu za ndani kwa maadui zetu. Hatujui tunapigana na nani.

Katika kazi yangu ya uandishi wa habari, nimezungumza na wadadisi wa maswala ya usalama na bwana Rais wengi wao wanahisi twapigana wenyewe kwa wenyewe. Na iwapo si wenyewe kwa wenyewe basi twafukuzana na kivuli cha fimbo ambacho hakisitiri jua.

Badala ya kuua magaidi tunajiua wenyewe kwa wenyewe. Kwa kweli hatuwezi shinda vita hivi ikiwa twaumizana wenyewe kwa wenyewe badala ya kuungana. Mara tunaambiwa ni MRC, mara ni Mungiki, mara magaidi, maragodoro na sasa waziri wako Ole Lenku ana mapya zaidi.

Waswahili wanasema “Bata ata umlishe mawe bado atahara”. Bwana Rais, tumwamini nani?

Bwana Rais, majuzi uliingia na taswira mpya kabisa katika uwanja wa Nyayo; magari ya kujikinga na risasi na usalama zaidi. Hii, si kawaida tangu uongozi wa Hayati Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Toroitich arap Moi na Mwai Kibaki. Iwapo wewe unahofia, je sisi walalahoi tutahisi vipi?

Mauaji ya Mpeketoni ni sawia nay ale ya Tana River. Damu ya wana Mpeketoni inalilia haki. Kina mama wamechwa bila watoto na waume huku watoto wakisalia mayatima kwa kosa la serikali walilolichagua ki katiba, serikali iliyowaahidi kuwalinda pamoja na mali zao. Mauaji ya kiholela yanazidi kugonga vichwa vya habari, baadhi ya walinda usalama wameamua wao ndio majaji na mawakili kwa Wakenya wanyonge wasio na mtetezi.

Bwana Rais, wakenya wanalia; kuanzia Easatleigh, Baragoi hadi Mandera.

Nina machungu na mengi ya kukueleza lakini muda hauniruhusu. Kumbuka Kenya ni jina, nchi ni sisi.

Ni hayo tu kwa sasa.

Shukran.

{youtube}1fZJZrcxKNI{/youtube}

About this writer:

Jeff Omondi (Writer)