Shigongo Adai Diamond Hawezi Kuwa Staa Milele

Mkurugenzi wa Global Publishers na mwandishi maarufu wa vitani Erick Shigongo ameibuka na kudai kuwa staa wa muziki wa Bongo fleva Diamond Platnumz hawezi kukaa kwenye chati kwa muda mrefu.

Shigongo ameweka wazi kuwa katika sanaa kuna kubadilishana nafasi kwaiyo pamoja na kwamba Diamond yuko juu kwa sasa lakini atakuja kuondoka na wataakaa wasanii wengine.

Kauli hiyo ya Shigongo ilikuja baada ya kuulizwa swali wakati akifanya mahojiano na Global TV Online iwapo alishawahi kumsaidia jambo lolote Diamond kwani staa huyo amemtaja Shigongo kama mmoja wa ‘role model’ (mtu aliyempa hamasa ya mafanikio) wake.

Sikumbuki kama nilishawahi kumsaidia, watu wananiambia lakini mimi sina kumbukumbu, labda kuandikwa magazetini kwa ajili ya promosheni za kazi zake za muziki, pengine kutokana na nasaha zangu ambazo huwa nazitoa kuwashauri Watanzania wenzangu na kuwapa mbinu za kujikwamua kwenye umaskini.

Ninachoweza kumwambia tu ni kwamba apambane.  Unajua ukifanikiwa unapata marafiki wengi, na wengi wao wanakuwa wanataka pesa zako au cheo chako, siku pesa zikiisha hutowaona tena. Ametoka kwenye umaskini, asisahau alikotoka.

Walikuwepo akina Mohamed Ali, wakaondoka, wakaja kina Tyson, wakaondoka, sasa hivi yupo Maywether, ataondoka atakuja mwingine. Mimi nipo, nitaondoka.   Je, nikiondoka watoto wangu wataendelea kula chakula kilekile? Watasoma shule zilezile? Lakini pia tulikuwa nao akina Mr. Nice, waliondoka, sasa hivi yupo Diamond, itafika wakati ataondoka, watakuja wengine, hatakuwa championi milele.

Ninachoweza kumwambia ni kwamba  awekeze kwa ajili ya baadaye, ukiwapelekea watu chakula sehemu uliyotoka, Tandale,  watasema unatafuta kiki, ukila peke yako Madale watasema huyu jamaa mbinafsi, mimi namshauri asisikilize watu wanasema nini, aendelee kupambana hadi mwisho”.