Kala Jeremiah na Ndoto Ya Kujenga Shule Kwa Ajili Ya Yatima na Watoto wa Mitaani

Msanii wa muziki wa hip hop nchini Kala Jeremiah ameibuka na kuweka wazi mipango yake ya kujenga shule ambayo itawasaidia Watoto yatima na Watoto wa mitaani.

Kala amefunguka na kusema kwa muda mrefu imekuwa ni ndoto yake kufanya kitu kikubwa kama hicho ili aweze kuwasaidia Watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wasiojiweza.

Kwenye mahojiano yake aliyofanya na Millard Ayo, Kala Jeremiah ameongea haya kuhusu mpango Wake huo kabambe:

Nina Ndoto ya kujenga shule kubwa ambayo watasoma watoto yatima bure, itakuwa boarding school kubwa sana ambayo pia itahudumia watoto wote wanaoishi katika mazingira magumu na nikitimiza ndoto yangu hiyo hata Mungu akinichukua baada ya hapo nadhani nitakuwa nashangilia”.

Kala Jeremiah amekuwa mmoja kati ya wale wasanii ambao wamekuwa wakifanya muziki wa kuleta tija ambao unajikita katika kugusa mambo muhimu katika jamii.

Kala Jeremiah Akana Kuwa na Bifu na Roma

Msanii mkongwe wa Bongo fleva anayefanya miondoko ya kuchana Kala Jeremiah amekana kabisa tetesi zinazodai kuwa ana bifu na Msanii mwenzake Roma Mkatoliki.

Habari za wasanii hao kuwa na bifu zilianza baada ya wasanii hao kupunguza ukaribu waliokuwa nao zamani na hata kutopeana sapoti katika kazi zao Ikiwa ni pamoja na kutopostiana Kwenye mitandao ya kijamii.

Kwenye mahojiano aliyofanya na Ijumaa Wikienda, Roma amedai kuwa hana bifu lolote na Roma bali ni marafiki wazuri bado:

Hapana sina bifu na R.O.M.A yeye kwangu ni kama ndugu na hatuna tofauti zozote zile na sina background hasa ishu hiyo iliibukia wapi.

Hatuna bifu. Kwanza R.O.M.A kwa sasa ana kundi, kwa hiyo muda mwingi unakuta anafanya mambo yake na kundi lake. Hatuambatani tena ni kama ambavyo unaweza usimuone R.O.M.A na ndugu yake yeyote wakimbatana, lakini ukamuona na Stamina. Utasema haelewani na ndugu zake? Kuna muda tunaonana na mambo mengine yanaendelea, lakini si kwamba tuna tofauti. Kuhusu mitandaoni, ukitazama Instagram, kwanza ni kama hayupo vile, kwa hiyo tupo sawa”.

Lakini pia Kala alicheka baada ya kusikia tetesi kuwa eti hawaelewani sababu ya penzi la Dayna Nyange ambapo amesisitiza kuwa wapo vizuri tu.

Kala Jeremiah Ameongea Haya Baada ya Kumwagiwa Sifa Kibao na Makamu Wa Rais

Mwanamuziki wa Bongo fleva anayetumia miondoko ya kuchana hip hop, Kala Jeremiah amesema kuwa alipokea kwa mshtuko taarifa za kusifiwa na makamu wa raisi.

Wiki iliyopita Makamu wa Raisi Mama Samia Suluhu Hassan alimsifia Kala Jeremiah kwa nyimbo yake mpya inayoitwa ‘kijana’. Mama Samia alifunguka hayo kwenye kikao cha CCM kilichofanyika Dodoma ambapo alikuwa anawaasa wasanii wa Bongo fleva kuimba nyimbo za kuhamasisha na kufundisha jamii.

Ambapo kwenye hotuba yake hiyo alidai kuwa ni vyema wanavyotoa nyimbo kama ‘Natamba; ya Aslay na watu wanazipenda lakini umefika wakati wasanii watunge nyimbo kama ya Kala Jeremiah ‘kijana’ ambayo inawaasa vijana wenzake kufanya kazi kwa bidii na juhudi zote ili tu waweze kujenga taifa.

Baada ya kumwagiwa sifa hizo mbele ya waandishi wa habari wote Kala amefunguka haya ili kuelezea ni jinsi gani alijisikia na anachukulaje heshima hiyo aliyopata kutoka kwa kiongozi mkubwa serikalini;

Nilipigiwa simu na watu mbali mbali kuwa nimepata pongezi kutoka kwa makamu wa raisi kwangu mimi ilikuwa ni mshtuko mkubwa sana na ni kitu kikubwa sana kwa msanii yoyote yule kutamkwa hadharani ilikuwa ni heshima kubwa sana kwangu na imenifanya nione kuwa nina deni kubwa sana la kuendelea kupigana kwenye kuendelea kuiongelea jamii na kuendelea kuwaongelea wale  watu ambao hawana sauti na imenipa nguvu ya kuendelea kufanya kile ninachoendelea kufanya”.

Kala ni moja kati ya wasanii wachache nchini aliyejipatia umaarufu kwa kuimba nyimbo za siasa na nyimbo ambazo zinagusa matatzo ya kijamii tofauti na wasanii wengine ambao huimba mapenzi na vitu vingine vya tofauti.

 

Kala Jeremiah Ameandika Barua Ya Wazi Kwa Watanzania Wote Juu Ya Dr. Luis ‘900 itapendeza’

Mwanamuziki wa Bongo fleva kwa miondoko ya kurap Kala Jeremiah amewaasa Watanzania wote wampende na kumthamini Dk Luis Shika au maarufu kama ‘900 itapendeza’ kwani mzee huyo ni mpango wa Mungu na Baraka kutoka kwa Mungu wetu sisi Watanzania.

Mzee huyo alipata umaarufu baada ya kununua nyumba tatu kwenye mnada na kushindwa kuzilipia kwani baada ya polisi kumpiga sachi hawakumkuta na hata senti mfukoni hali iliyopelekea kupelekwa rumande. Kwa kupitia ukurasa wake wa Instagram Kala alifunguka mazito juu ya mzee huyo:

Nimesikiliza kwa makini sana maelezo ya mzee wetu sitaki kuongelea utajiri wake wala umaskini wake nataka kuongelea majaribu aliyokutana nayo katika safari yake ya maisha. Ni wazi kabisa kuwa mzee huyu yupo duniani kwa kuwa Mungu kamchagua na Mungu humchagua mtu kwa kusudi lake. Nionavyo mimi Mzee huyu ni baraka kutoka kwa Mungu haijalishi madhaifu yake ila kwa uhakika ni mpango wa Mungu kuwepo kwake kwetu. Niwaombeni wanajamii tumuonee huruma na tumpende hicho ndicho kitu pekee anachohitaji mzee huyo na kwa hakika amekikosa kwa miaka mingi haitakugharimu chochote kumuhurumia na kumpenda, nawaomba”.

Tangu jambo hili litokee wiki iliyopita Dkt. Shika amekuwa mtu mmoja maarufu ambaye amekuwa akifuatwa na waandishi wa habari kila kona anayoenda na kupelekea kuwa kivutio mtandaoni kote.

Kala Jeremiah Atangaza Nia Yake Ya Kuwa Mbunge na Kuingia Ikulu

Mwanamuziki wa Bongo fleva na rapa mkongwe anayefanya vizuri bado kwenye gemu Kala Jeremiah amefunguka kuhusu nia yake ya dhati kabisa ya kugombea ubunge kwa mwaka 2020 na malengo yake ya kuingia ikulu hapo baadae.

Kala ni moja kati ya wasanii ambao ni wazalendo kwani nyimbo zake nyingi zimelenga katika kuimba kuhusu mambo siasa hasa mambo ambayo yanaendelea katika jamii yetu hivi sasa. moja kati ya nyimbo zake ni Dear God, na hivi karibuni ametoa nyimbo yake inayoitwa ‘kijana’ ambayo kama kawaida yake tofauti na wasanii wengine ambao wamejikita katika kuimba mapenzi Kala ameegemea upande wa maendeleo ya kijamii.

Kwenye mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni Kala alifunguka kuhusu nia yake ya kuingia kwenye siasa na sio tu kuimba siasa kutokana na upendo na uzalendo;

Mimi tayari nimekuwa mbunge kwa miaka mingi nimeshakuwa mbunge toka 2007 toka nilipotoa wimbo wangu unaoitwa ‘wimbo wa taifa’  kwani watu wengi waliniita mwanaharakati, mbunge, mtetezi wa haki za wanyonge kwangu mimi hapo mbunge kwaiyo kwa sasa kama nitaingia kwenye siasa nitaangalia sana kwenye kuwa raisi kwaani naamini kwamba mimi ni mwanasiasa tayari na nikiwa raisi ntashiriki katika kusukuma hili gurudumu la nchi nzima kwani ninao uwezo wa kuiongoza nchi na pia ninayo maono mazuri ya kupeleka nchi hii sehemu nzuri zaidi “.

Kala aliendelea kufunguka kuhusu uongozi uliopo sasa;

Mheshimiwa Raisi nampenda tokea zamani nilikuwa naona kama anawea kuwa kiongozi mzuri ila leo hii nikipata nafasi ya kumshauri leo hii ntamshauri kwamba tulikuwa tunaimba kuhusiana na ufisadi lakini sahivi naona anapigania sana ufisadi, sahivi nitakachomuomba mimi ni uhuru wa kujieleza ntamuomba na hela kwenye mifuko ya wananchi ambao ni mashabiki zangu”.

 

Kala Jeremiah Amuongelea Tundu Lissu

Mwanamuziki wa hip hop Kala Jeremiah amefunguka kuhusu kisa kilichotokea kwa mwanasiasa na mbunge wa Chadema Tundu Lissu.

Kala ambaye ni mmoja wa wasanii wa hip hop ambaye anapenda kuimba mambo ya siasa katika nyimbo zake kama Dear God, wimbo wa taifa na nyinginezo amesema unyama uliofanywa kwa Tundu Lissu umemshtua na kumshangaza kama ilivyokuwa kwa mtanzania yoyote.

Kala Jeremiah amefunguka;

Kile kitendo alichofanyiwa Tundu Lissu lilinishtua ni tendo baya sana kwa nchi yetu kwa sababu hatujawahi kuzoea hivyo vitu unajua kuna nchi ambazo wakisikia jambo kama hilo wanaona kama kitu cha kawaida lakini kwetu lilishtua kila mtu aliye na akili timamu alishtushwa sana na habari hizo”.

Kala aliendelea kusema:

“Kile kitendo kinapeleka ujumbe mbaya kwa nchi nyingine kuhusiana na nchi yetu kwani kitu pekee ambacho nchi yetu inajivunia siku zote ni amani kwaiyo kitendo hicho kimeleta dosari sana, yapo matukio mengine lakini hilo ni tukio la kuhuzunisha sana”.

Kala Jeremiah aliyekuwa amekaa kimya kwa muda amerudi kwenye gemu na hivi sasa ana wimbo mpya unaoitwa ‘Kijana’.

Wasanii wengi wamekuwa waoga kuzungumzia siasa au hata matukio yanayotokea nchini Kama shambulizi la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu hasa ukizingatia msanii kama Roma alitekwa kutokana nakuongelea mambo yanayoendelea nchini, lakini wanaharakati kama Kala hutoa nyimbo za kuelimisha na kuhimiza mabadiliko katika jamii kwa hiyo Big up kwa Kala.